Mkataba wa kuidhinisha madaktari watiwa saini

Katibu Mkuu wa KMPDU Ouma Oluga katika kikao cha wanahabari cha awali. [Radio Maisha]

Madaktari 100 kutoka Cuba wanatarajiwa kuwasili nchini tarehe 28 mwezi huu. Mkataba utakao waidhinisha madaktari hao nchini umetiwa saini na Baraza la Magavana na Wizara ya Afya.

Akizungumzia mkataba huo, Mkurugenzi wa Kamati ya Kaunti ya Tharaka Nithi, Dakta Gichuyia Nthuraku ametetea hatua hiyo akisema madaktari hao watakuwa tu wasaidizi wala hawaji kuchukua nafasi za madaktari wa humu nchini.

Gichuyia amesema madaktari hao watatumwa mashinani ambako kuna upungufu wa madaktari. Vilevile amesema changamoto kuu ni kuwa baadhi ya madaktari nchini hukataa kufanyia kazi mashinani.

Ikumbukwe Muungano wa Madakatari, KMPDU umepinga vikali hatua hiyo ukisema taifa lina takribani madaktari 1, 200 ambao hawajaajiriwa.

Wiki iliyopita katika mkutano wa pamoja, KMPDU na Chama cha Wahadhiri UASU zilisema iwapo serikali haitatekeleza matakwa ya wahadhiri, miungano yote ya wafanyakazi nchini itapanga mgomo wa kitaifa utakaolemaza huduma zote nchini.